HAYA NDIYO MAAMUZI YA MWISHO YA ‘CANNAVARO’ KUHUSU STARS
Nahodha wa zamani wa ‘Taifa Stars’ Nadir Haroub ‘Cannavaro’ amesema hatoripoti kambini kujiunga na kikosi cha Mkwasa kinachojiandaa na mchezo wa kirafiki wa kimataifa dhidi ya Kenya kisha mchezo dhidi ya Misri kuwania kufuzu kucheza fainali za mataifa ya Afrika.
Cannavaro amesema anafurahi jinalake kuwepo kwenye orodha ya wachezaji wa timu ya taifa lakini hawezi kujiunga na timu kwasababu tayari amesha-staafu kuichezea Stars.
“Nimepata taarifa jinalangu limetajwa kwenye kikosi cha timu ya taifa, nimefurahi lakini siwezi kujiunga na timu kambini kwasababu tayari nimeshataafu kuichezea stars”, amesema mlinzi huyo wa kati wa Yanga nilipofanya nae mahojiano mafupi mara baada ya kumalizika mchezo wa fainali ya FA Cup na timu yake kuibuka bingwa.
“Namuheshimu sana kocha Mkwasa kwa kuniita kwenye timu, lakini mimi tayari nilishakabidhi barua yangu TFF ya kustaafu kuichezea timu ya taifa na huo ndiyo msimamo wangu wa mwisho”.
Cannavaro alitangaza kustaafu kuichezea timu ya taifa ya Tanzania baada ya kocha Mkuu wa timu hiyo Charles Boniface Mkwasa kumtanga Mbwana Samatta kuwa nahodha mpya wa Stars kitendo ambacho Cannavaro alikilalamikia kwamba yeye hakupewa taarifa rasmi.
Beki huyo ambaye ameitumikia Stars mfululizo kwa zaidi ya miaka 10 alidai kwamba, alipata taarifa za kocha kumbadilishia majukumu kupitia vyombo vya habari hivyo hakuona kama ilikuwa ni sahihi, siku chache baadaye akatangaza kustaafu kuitumikia Stars.
No comments: