Header Ads


Breaking News
recent

Mbeya City yaifunika Simba





KUNA vitu vitatu vinaendelea kwenye Ligi Kuu Bara. Kuna timu zinawania ubingwa, nyingine nafasi ya pili na nyingine zinapambana kuhakikisha hazishuki daraja.
Mbeya City imekomaa kwenye nafasi ya tatu imeziba njia Simba isiipate nafasi hiyo au hata kupenya kuelekea nafasi ya pili. 
Mbeya City ambayo inafurahia nafasi hiyo kwa vile ni msimu wake wa kwanza katika ligi hiyo, imeifunika Simba ambayo ni mpinzani wake wa karibu sasa, kwa kushinda mechi nyingi ugenini.
Kwenye msimamo wa ligi, Mbeya City ina pointi 42, mbili tu nyuma ya vinara Azam wenye pointi 44 na Yanga ikiwa nafasi ya pili na  pointi 43. 
Timu hiyo inayomilikiwa na Halmashauri ya Jiji la Mbeya imeshinda mechi sita kati ya mechi 12 ilizocheza ugenini huku ikitoka sare mara nne na kupoteza michezo miwili. Ilipoteza mchezo dhidi ya Yanga 1-0 na Coastal Union 2-0.
Simba inayoshika nafasi ya nne ikiwa na pointi 36 (kabla ya mechi za jana Jumapili) imeshinda mechi tatu kati ya kumi ilizocheza ugenini huku ikitoka sare mara nne na kupoteza mchezo mmoja. Ilifungwa 1-0 na Mgambo JKT Jijini Tanga.
Mbeya City pia imeizidi Simba kwa mabao ya kufunga kwenye mechi ilizocheza ugenini kwani imefunga jumla ya mabao 17 huku Simba wakiwa na mabao 12 kwenye mechi za aina hiyo.
Mbeya City kwa sasa imebakiza mchezo mmoja tu ugenini dhidi ya Ashanti United huku Simba ikiwa na mechi dhidi ya Kagera Sugar ya ugenini Bukoba, Azam na Yanga ambazo itakua ugenini ingawa  zitachezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Katika hatua nyingine, Mbeya City imedai kwamba uamuzi wao wa kuanza kutumia usafiri wa basi katika mechi za hivi karibuni hauna maana kwamba wamefilisika, bali walikuwa na muda mwingi wa kujiaanda. Imesema inapoamua kutumia usafiri wa ndege, huzingatia  umbali wa inapokwenda kucheza na ugumu wa mechi.
Kuhusu mechi ya Prisons, Katibu Mkuu wa Mbeya City, Emmanuel Kimbe, alisema: “Mechi yetu na Prisons ni muhimu na ni ngumu kuliko mechi zilizopita kwani wao kwetu ni kama ilivyo kwa Simba na Yanga kwa Dar es Salaam.
“Sisi tuna ushirikiano nao endapo timu moja inacheza na nyingine,  lakini tunapokutana ushirikiano huo haupo. Hatutaitoa timu mjini itaendelea na maandalizi yake hapo hapo, lakini tutafanya jitihada za kuhakikisha tunapata ushindi, kwani Simba wakishinda mechi yao na Coastal na sisi tukipoteza lazima watachukua nafasi yetu na sisi hatutaki kuwaachia Simba.”
Simba kabla ya mechi yao na Coastal Union jana Jumapili jioni ilikuwa inashika nafasi ya nne kwa kuwa na pointi 36.

No comments:

Lazaro Masika. Powered by Blogger.